Salman Mfursi alikuwa mmoja wa masahaba wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Kama sahaba wa Mtume, alikuwa maarufu zaidi miongoni mwa waliokuwa maarufu. Lakini simulizi za maisha yake, kinyume na simulizi za maisha ya wengi wa masahaba wengine wa Mtukufu Mtume, (s.a.w.w.) zimefichika katika fumbo. Ni kidogo sana kinachojulikana kuhusu simulizi hizo. Hii ni ajabu, ukichukulia hadhi yake kubwa mbele ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) - bwana wake katika dunia hii na akhera - na kujiweka kwake katika hali ya shauku kubwa na Uislalmu. Matukio ya niaisha yake, inaelekea yanasubiri mtafutaji ukweli wa siku zijazo, kuja kuyafichua.
Jaribio la wastani limefanywa katika kurasa za kitabu hiki katika kuelezea maisha ya Salman Mfursi kutoka kwenye vyanzo ambavyo vinapatikana bila shida. Jaribio hili linalenga kwenye mapenzi yake juu ya Allah (swt), kutafuta kwake bila ya kuchoka, ukweli wa milele; “ugunduzi” wake wa Uislamu na utii wake juu yake; na ufuasi wake kwa Muhammad Mustafa, Mtume wa Allah (s.a.w.w.); na “mfungamano” wake na Haki usiotenguka, Ukweli na Unyofu.
Kisa cha Salman ni sehemu muhimu ya urithi wa Uislamu wa utiifu na msukumo, na ni utafiti mkali juu ya mwenendo ambamo alionyesha utekelezaji wa kanuni za Uislamu kwenye maisha binafsi na ya kijamii. Alikuwa ni shahidi, kwa kiwango cha juu kabisa wa Ukweli na utukufu wa kanuni hizo. Yeye alitoa pia mchango mkubwa na wa kuvutia sana kwenye maelezo ya utambuzi na uzoefu wa kidini wa wanadamu wote.
Allah amuwie radhi mtumwa wake mpendwa, Salman Mfurusi. Alidhihirisha utii wake kwa Allah (swt), na ufuasi wake kwa Muhammad Mustafa (s.a.w.w.).